Kipi Sijasikia ![1]()
Siku moja niliwahi kuketi kitako na rafiki yangu fulani tukijadili safari ya ubinadamu. Ni mambo gani mtu hupitia mpaka kufikisha umri japo wa miongo minne tu hapa duniani? Nakumbuka tulijadili mpaka jua lilipokuwa linazama kuashiria kwamba kiza kinaelekea kutanda na kuanza kuikaribisha siku mpya. Jambo moja lililokuwa wazi katika mjadala ule na rafiki yangu ni kwamba binadamu hupitia mengi. Ndio maana unaambiwa kila mtu anayo simulizi ya kuvutia. Kinachotutofautisha ni kwamba wengine wanajua kuhadithia kuliko wengine. Ndio maana kuna vitabu,muziki, filamu nk.
Miongoni mwa mapito ya binadamu ni pamoja na kusemwa sana. Upende usipende,utasemwa. Kama sio jirani yako basi ni yule jamaa anayejiita “rafiki yako”.Ukiwa maarufu ndio kabisaaa. Kila unalolifanya ni mali ya midomo ya watu. Na katika zama hizi ambapo mtu anaweza tu kujipa jina na kuifanya computer au simu yake kuwa “ngao”,basi ni vyema tu kutambua kwamba wanaopenda kuongea wamewezeshwa zaidi.
Professor Jay ni mwanamuziki nguli. Ni mkongwe katika sanaa ya burudani nchini Tanzania. Ni maarufu.Haishangazi basi kuona kwamba ashasemwa sana. Ungedhani katika kusemwa yapo ambayo hajayasikia.La! Anasema yote anayasikia ila anaamua tu kusonga mbele. Pengine hilo ndilo la msingi na ambalo sote[maarufu na wenzangu na mie] tunapaswa kufanya.Ukisemwa na kusikia,sikiliza.Songa mbele.
Huu hapa ni wimbo mpya kutoka kwa Professor Jay akimshirikisha Diamond Platinumz.Unaitwa Kipi Sijasikia. Ni production ya Bongo Records chini ya P-Funk Majani.